TFF Kujadili Kauli ya Serikali Kufuta Katiba Yake, Kocha wa Azam Afungiwa
Rais wa TFF, Leodger Tenga
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepokea
barua ya Serikali ikielezea uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutengua uamuzi wa Msajili
wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kuidhinisha marekebisho ya Katiba
ya TFF toleo la 2012.
Baada ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25 mwaka huu),
Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye ameagiza
kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko hilo.
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2
mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
KOCHA Mkuu wa Azam, Stewart John Hall amefungiwa
mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushusha bukta yake na
kumlalamikia mwamuzi msaidizi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) kati ya timu yake na Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za
michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013
inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali.
Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira
ametozwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye
mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja
wa Manungu.
Ally Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro naye
ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000
baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya
juu. Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar
iliyochezwa Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia
ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini
Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea wachezaji
wa timu yake wacheze rafu.
Naye Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho
amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya
mechi dhidi ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa
Mabatini mjini Mlandizi. Pia Kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie
amepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa
lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya
mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa miezi
sita.
Vilevile timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa
kufika uwanjani kwenye mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7
mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es
Salaam.
Pia Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki
wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa
mechi yao dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu
yake kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa
mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu ya Burkina Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000
kutokana na kuonesha vitendo vya ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya
Mbeya City iliyochezwa Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro.
Faini ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada
ya kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa
Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki
wake kumtolea lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Morogoro (MRFA), Hamis Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa
mezani katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao kuchelewa
kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi
(Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto
Africans, Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi
Dodoma, JKT Kanembwa, Moro United.
Mchezaji Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal
Union alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa
timu ya Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema
aliruka uzio na kwenda kupigana na washabiki.
No comments:
Post a Comment