MKATABA WA AMANI CONGO WASAINIWA.
MKATABA wa kumaliza vita mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo leo umetiwa saini mjini Addis Ababa-Ethiopia na
viongozi wa nchi za Maziwa Makuu. Viongozi wa nchi za maziwa makuu leo
mjini Addis Ababa wameutia saini mkataba wa kumaliza vita mashariki mwa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo uliofikiwa kwa upatanishi wa Umoja wa
Mataifa.
Viongozi hao walishindwa kuutia saini mkataba huo mwezi uliopita
kutokana na mzozo juu ya nani anapaswa kukiongoza kikosi cha kulinda
amani kitakachowekwa mashariki mwa Jamhuri ya Kongo.
Kutiwa saini kwa mkataba huo kutawezesha kuundwa kwa kikosi maalum
cha jeshi la Umoja wa Mataifa kitakachoweza kuingilia kati katika eneo
hilo la mashariki mwa Kongo na kupambana na waasi pamoja na kuanzisha
juhudi mpya za kisiasa. Viongozi walioutia saini mkataba huo mjini Addis
Ababa ni wa Msumbiji, Rwanda, Tanzania, Afrika Kusini, Kongo, Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Kongo na Sudan ya Kusini.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Nesirky ameeleza kuwa Umoja wa Afrika,
mataifa 11 ya eneo la maziwa makuu, (ICGLR)pamoja na jumuiya ya
wanachama 14 ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC,watakuwa “wadhamini
wenza”.
Umoja wa Mataifa unatarajiwa kumteua mjumbe maalum atakaefuatilia
utekelezaji wa makubaliano hayo. Maofisa wa Umoja wa Mataifa wamesema
kuwa hali ya kutokubaliana mwezi Januari ilitokana na wasi wasi juu ya
taratibu, lakini sio kutokana na maudhui ya mkataba. Jason Stearns,
mchambuzi anaefuatilia masualaya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, mapema
mwezi huu aliyaita makubaliano hayo kuwa ni “hati isioeleweka kabisa.”
Amesema makubaliano hayo, yanalenga katika vipengere
vitatu:”kuyazuwia mataifa ya eneo husika kujiingiza katika masuala ya
ndani ya nchi nyingine, kuhimiza kufanyiwa mageuzi kwa taasisi dhaifu
nchini Kongo na kuvutia uratibu bora zaidi wa wafadhili na ushiriki wao.
Eneo la mashariki mwa Kongo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini
limevurugwa na makundi kadhaa yenye silaha katika muda wa miongo miwili
iliyopita, huku makundi mapya ya waasi yakizuka kila mara, baadhi yao
yakiungwa mkono na nchi jirani.
Ongezeko la hivi karibuni la machafuko lilitokea mwaka 2012 na
kusababisha kuzuka kwa kundi la waasi la Machi 23, (M23) ambalo kwa muda
liliuteka mji muhimu wa Goma Novemba mwaka jana. Kundi la M23 liliundwa
na wapiganaji wa zamani wa kundi la waasi wa kabila la Watutsi ambao
hapo awali waliingizwa katika jeshi rasmi la Serikali ya Congo kwa
mujibu wa makubaliano ya amani, lakini wanadai kuwa masharti ya
makubaliano hayo hayakutimizwa.
Mungu inua mkono wako na ulete amani huku.AMEN
Mungu inua mkono wako na ulete amani huku.AMEN



No comments:
Post a Comment